Ijumaa, 18 Oktoba 2013

`Ondoeni urasimu mikopo ya vijana`

15th October 2013

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel.


Serikali imezitaka halmashauri za wilaya, manispaa na majiji, kuondoa urasimu katika kuwahudumia vijana wanapohitaji taarifa kuhusu upatikanaji wa mikopo na huduma nyingine.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel, alitaka halmashauri kutoa taarifa sahihi zitakazowasaidia vijana kupata mikopo kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Alikuwa akizungumza na watendaji wa Sekretarieti ya Mkoa na wakuu wa idara za halmashauri za Mkoa wa Arusha, mwishoni mwa wiki.

Alisema katika  halmashauri nyingi, kuna urasimu wa kutoa huduma na taarifa mbalimbali kwa wananchi na urasimu huo umekuwa ni kikwazo kikubwa kwa  vijana kupata habari ili washiriki kikamilifu katika kuimarisha miradi yao ya kiuchumi.

Alisema wapo baadhi ya watendaji katika halmashauri ambao hawasikilizi na kuwapatia majawabu sahihi wananchi kutokana na urasimu uliokithiri na akawataka kubadilika.

Alisema urasimu huo umesababisha vijana wengi kutokuwa na elimu sahihi ya kupata mikopo ili kuharakisha maendeleo na mageuzi ya kiuchumi vijana wengi wanakosa mikopo kutokana na urasimu uliopo kwenye halmashauri.

Alisema serikali imetenga Sh. bilioni 6.2 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana hapa nchini ambapo Sh. bilioni 1.34 zimetengwa kwa ajili ya kuwakopesha vijana wanaohitimu vyuo vikuu kwa ajili ya kuwasaidia kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Profesa Gabriel pia ameziagiza serikali za mitaa kuhakikisha zinaunda vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) kwa ajili ya vijana ambapo kupitia vikundi hivyo vijana watapata mikopo kwa urahisi kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Alisisitiza nidhamu ya matumizi ya fedha za mikopo na kusema kuwa mtaji mkubwa wa mafanikio ya maendeleo ya vijana, ni suala la uaminifu, uadilifu na uwajibikaji na kusisitiza kuwa hayo ni mambo ya msingi katika uendeshaji wa mfuko huo.

 

CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni