Tusikubali `wauza unga` kuichafua Tanzania ughaibuni
Taarifa kwamba kuna Watanzania 175 wanaoshikiliwa
katika magereza tofauti nchini China baada ya kukutwa na makosa
mbalimbali yakiwamo ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya si
nzuri kwa taifa letu. Zinaichafua Tanzania.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye aliyepewa taarifa hiyo ya kustusha
wakati alipotua China juzi kuanza ziara yake ya kikazi. Alihuzunishwa
sana.
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini China, Watanzania hao wamefungwa
katika maeneo mbalimbali ya China, yakiwamo ya Hong Kong, Macao na
China Bara.
Mbaya zaidi, waliokamatwa wala si watu wa jinsia moja, siyo vijana wa
kiume pekee kama ilivyozoeleka. Bali, wapo pia wanawake ambao idadi yao
ni kubwa sana kiasi cha kumshangaza hata Waziri Mkuu Pinda.
Alipokuwa akielezea suala hilo, Pinda alisema idadi ya watuhumiwa hao
kutoka katika nchi moja pekee, hasa yetu ya Tanzania, ni kubwa sana.
Inalitia aibu taifa hili ambalo wasifu wake kimataifa umekuwa ni wa
kupigiwa mfano kwa miaka mingi.
Sisi pia tunaamini kuwa idadi hiyo ni kubwa, hasa kwa kujua kuwa idadi
hiyo ni ya nchi moja tu ya China na haihusishi Watanzania wengine
wanaoshikiliwa katika mataifa kama ya India, Pakistani, Saudi Arabia na
kwingineko duniani.
Ni taarifa zinazoiharibia Tanzania sifa yake ya miaka mingi mbele ya
jumuiya za kimataifa, sifa ya kuwa taifa lenye watu walioshiba maadili
na hivyo kutohusika mara kwa mara na matukio ya uhalifu mkubwa kama wa
biashara ya dawa za kulevya.
Hakika, taarifa hizi zinateteresha heshima ya Tanzania. Zinaharibu
taswira nzuri mbele ya nchi rafiki kama ya China, ambayo ni miongoni mwa
washirika wetu wakubwa wa maendeleo.
Hakuna asiyejua athari za taifa changa kiuchumi kama Tanzania kukumbwa
na taarifa mbaya za uhalifu. Mojawapo ya athari hizi ni kushuka kwa
kiwango cha uaminifu. Kwa mfano, ni wazi kwamba sasa, maafisa wa usalama
katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini China watakuwa na ukaguzi wa
ziada dhidi ya raia watokao nchini mwetu.
Ni wazi vilevile kuwa hata wafanyabiashara wa Tanzania watakuwa na
wakati mgumu China kwani watalazimika kuwashawishi washirika wao
kibiashara kuwa wao ni watu safi na siyo miongoni mwa wauzao dawa za
kulevya.
Jambo hili linadhihirisha kuwa sasa hali ni mbaya. Kuna kazi kubwa ya
kufanya kuhakikisha kwamba aibu hii inakomeshwa na heshima yetu
inalindwa kwa nguvu zote.
Sisi tunatambua jitihada zinazochukuliwa na serikali katika mapambano
dhidi ya dawa za kulevya. Tunatambua vilevile mpango wa serikali wa
kutaka kuunda chombo maalum kitakachokuwa na nguvu zaidi kisheria,
kifedha, kiteknolojia na hata rasilimali watu katika kukomesha janga
hili. Ni hatua nzuri.
Hata hivyo, kama alivyosema Waziri Mkuu Pinda, tunadhani kwamba sasa
kuna kila sababu ya kuongeza nguvu katika kukabiliana na tatizo hili.
Uzoefu unaonyesha kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya si
watu wa kada ya chini. Wana ukwasi mkubwa na wamejipanga vya kutosha
katika kufanikisha mipango yao mbalimbali, ikiwamo ya kusafirisha
'mizigo' kutoka eneo moja hadi jingine.
Umma unapaswa kuelimishwa kila uchao kuhusiana na madhara ya dawa za
kulevya. Na hii inapaswa kuwa kampeni endelevu. Wananchi, hasa vijana
waelimishwe vilevile juu ya hatari ya kujihusisha na biashara hii.
Kwa mfano, waambiwe kuwa wanapokamatwa katika baadhi ya nchi kama
China, adhabu yake huwa kali ikiwa ni pamoja na vifungo virefu gerezani
au hata kunyongwa.
Ulinzi katika maeneo ya viwanja vya ndege uimarishwe. Watumishi
wanaohusika na ukaguzi katika maeneo hayo wapewe mafunzo zaidi ili
kukabiliana na mbinu mpya zinazoibuka kila mara za kupitisha 'unga';
wapewe vitendea kazi vya kisasa na pia wafuatiliwe kwa karibu ili kuona
kuwa hawapokei rushwa na kuwa sehemu ya mitandao hatari ya biashara za
dawa ya kulevya.
NIPASHE tunaamini vilevile kuwa njia nyingine nzuri ya kukomesha
biashara hii ni kuwafikisha mahakamani wale wote wanaokamatwa na pia
kuendesha upelelezi makini utakaorahisisha mchakato wa kupatikana kwa
haki mbele ya mkono wa sheria.
Shime, tukatae jina la Tanzania kuchafuliwa nje ya mipaka yetu kwa kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.