Tehama shuleni; Dhamira njema iliyokosa mikakati wezeshi
Kwa ufupi. Pamoja na dhamira njema ya Serikali kutaka
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutumika, mchakato wa ufundishaji na
ujifunzaji, imeshindwa kuandaa mazingira ya kuwezesha teknolojia hiyo
kufanya kazi katika shule za msingi na sekondari hasa zile za umma.
Soma kisa hiki; Mgeni anakuja nchini na kutaka pamoja na mambo
mengine kuwafundisha kompyuta watu wa jamii ya wafugaji ambao asili yao
ni maisha ya kuhamahama porini.
Mkutano unaitishwa na mkataba wa makubaliano
unawekwa kati yake na watendaji wa Serikali ili atoe elimu hiyo
vijijini. Baada ya mkutano sote tunashangilia.
Hadithi hii inashabihiana na yanayotokea sasa
katika sekta ya elimu nchini. Ilivyo ni kuwa baadhi ya mipango ya
kielimu haina tija kwa kuwa haitekelezeki, japo dhamira yake ni nzuri.
Kama haitoshi mipango hiyo siyo kipaumbele muhimu
kwa jamii licha ya ukweli kuwa imekuwa ikianzishwa kwa mbwembwe na ahadi
lukuki.
Tehama shuleni
Kilele cha maono duni ya wale waliopewa jukumu la
kusimamia elimu yetu, linajionyesha katika mipango iliyopo ya kutaka
zana za kisasa za Tehama zitumike katika kufundishia na kujifunzia
shuleni.
Mfano mzuri ni mpango wa hivi karibuni ambapo ,
Serikali kwa kushirikiana na kampuni za Vodacom na Samsung wameanzisha
mpango wa kuziunganisha shule za sekondari nchini na mkongo wa
mawasiliano wa taifa.
Hatua hiyo itatoa fursa kwa shule kutumia kompyuta zilizounganishwa na intaneti katika kufundishia na kujifunzia.
Hata hivyo, pamoja na dhamira hii njema, swali la
msingi ni je, shule hizo zina miundombinu tayari kwa kuunganishwa na
mkongo wa mawasiliano?
Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, hadi mwaka 2012 shule mbili za
msingi na tano za sekondari (wasioona) ndizo zilizokuwa zimenufaika na
mradi huo wa mawasiliano ya mkongo wa taifa kati ya maelfu ya shule
zilizopo nchini.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa shule za msingi
zilizonufaika ni Buigiri (Dodoma) na Kizega (Singida). Shule za
sekondari zilizonufaika mpango huo ni Ilula (Iringa), Mpwapwa (Dodoma),
Ilowola (Njombe), Tumaini na Lulumba (Singida).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni