Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kushoto), akizungumza na
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda kabla
ya kuanza kikao cha Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma jana.
Picha:Selemani Mpochi.
Mwenyekiti Bunge la Katiba nguvu kwa Migiro,Chikawe
Yadaiwa ni baada ya mambo kumemwendea vibaya Chenge
Waziri wa Katiba na Sheria,Dk. Asha-Rose Migiro.
Kampeni za makundi ya vigogo wanaopigana vikumbo
kugombea uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba zimechukua sura mpya,
baada ya kundi lililokuwa likimuunga mkono Mbunge wa Bariadi Magharibi
(CCM), Andrew Chenge kudaiwa kubadili ghafla mwelekeo wa kampeni zake.
Habari za kuaminika zilizopatikana mjini hapa jana zilieleza kuwa kundi
hilo lililokuwa likimtaka Chenge, sasa linataka nafasi hiyo iwaniwe na
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro au Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Hatua hiyo inadaiwa kuchukuliwa na kundi hilo baada ya kubaini
kuongezeka kila uchao kwa nguvu za Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, ambaye tayari ameshatangaza kuwania nafasi
hiyo, huku zile walizozitarajia kutoka kwa Chenge zikizidi kushuka.
Habari hizo zinaeleza kuwa uthibitisho wa hilo, ni ujasiri ulioonyeshwa
na Sitta aliyeamua kutangaza hadharani azma yake ya kuwania nafasi
hiyo, huku Chenge akishindwa kuthibitisha kuwa atagombea ama la.
Uchaguzi wa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba unatarajiwa kufanyika
Jumapili wiki hii baada ya Bunge hilo kupitisha azimio la kuipitisha
rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu kesho.
Awali, Chenge aliiambia NIPASHE kuwa hayuko tayari kutangaza kama
atagombea nafasi hiyo au la kwa kuwa kanuni za Bunge hilo bado
hazijatungwa.
Kauli kama hiyo iliwahi pia kutolewa na Waziri Sitta katika siku hiyo hiyo, ambayo Chenge aliashiria kusubiri kanuni.
Hata hivyo, siku chache baadaye, hata kabla ya rasimu ya kanuni hizo
haijapitishwa na Bunge, Waziri Sitta alitangaza azma yake ya kugombea
nafasi hiyo kwa maelezo kwamba, anataka kutimiza ndoto ya Rais Jakaya
Kikwete ya kupata katiba bora.
Jumatatu wiki hii, Chenge alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana
kinyang'anyiro hicho, alikataa kuzungumza na badala yake akamtaka
mwandishi aendelee na shughuli zake.
Waziri Chikawe alipotafutwa na NIPASHE jana kuzungumza kama ana nia ya
kugombea nafasi hiyo au la, alimtaka mwandishi kuvuta subira kwa kuwa
wakati huo hakuwa na nafasi ya kuzungumza.
Dk. Migiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN) hakupatikana
kuzungumzia suala hilo.
Jitihada za kuwatafuta viongozi hao wanaotajwa kuwania nafasi hiyo zinaendelea.